Log inLog Out
For YouNewsEntertainmentRelationshipLifestyleSportTechnology
Msafara wa JPM waibua madudu

Romana Mallya

July. 31, 2020

Sambamba na hayo, pia alishtushwa kuelezwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo hana gari, magari ya kubebea wagonjwa ni bovu. Kutokana na matatizo hayo, ameagiza uchunguzi kufanyika huku akiwataka baadhi ya mawaziri kufika wilayani humo ili kujua chanzo cha matatizo hayo.
Magufuli alikumbana na mambo hayo jana alipokuwa njiani kwenda Dar es Salaam akitokea Lupaso, Masasi mkoani Mtwara alikokwenda kuongoza maziko ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, yaliyofanyika juzi.
Katika msafara huo, Rais Magufuli alisimama katika maeneo mbalimbali kusalimia wananchi na kuzungumza nao pamoja na kusikiliza kero mbalimbali. Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni Somanga, Kilwa mkoani Lindi, Ikwiriri na Utete wilayani Rufuji na Mkuranga mkoani Pwani.
Alipofika Ikwiriri alibaini kuwa kituo cha afya hakina gari la kubebea wagonjwa na alipohoji aliambiwa kwamba ni bovu pamoja na maeneo mengine ya wilaya hiyo.
Mmoja wa wananchi alimweleza Rais kuwa wilaya nzima haina gari la kubeba wagonjwa na kwamba yote ni mabovu na wanategemea ya wilaya ya Kibiti, iliyoanzishwa miaka kadhaa iliyopita baada ya kugawanywa kwa wilaya ya Rufiji.
Baada ya kuelezwa kero hiyo, aliwahoji viongozi wa eneo hilo akiwamo Mkuu wa Wilaya, Juma Njwayo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ambao kwa nyakati tofauti walitolea ufafanuzi.
Kaimu Mkurugenzi alisema halmashauri ina magari manne ambayo ni mabovu lakini si kwa kiasi cha kushindwa kufanya kazi. Alisema gari la Ikwiriri liko katika matengenezo na tayari wameshatenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Baada ya maelezo hayo, Rais alitaka kujua kama kaimu mkurugenzi huyo ana gari na kubaini naye hana na mkurugenzi ambaye yupo safarini jijini Dar es Salaam analo ingawa nalo lina matatizo.
Rais Magufuli alielezwa kuwa katika wilaya hiyo mwenye gari ni Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) lakini viongozi wengine hawana na Mkuu wa Wilaya hutumia hilo la DAS.
Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alishangaa kwa nini tatizo hilo lipo licha ya wilaya kukusanya mapato lakini gari la kubeba wagonjwa ni bovu.
Njwayo alisema gari alilokuwa akilitumia limetembea zaidi ya kilometa 300,000 na kwamba mwezi mmoja baada ya kuteuliwa alipata nalo ajali na kufanyiwa matengenezo yaligharimu Sh. milioni 28 na baada ya muda likasimama.
Kutokana na maelezo hayo Rais Magufuli alisema amesikia na kuyaelewa matatizo yote na kuahidi kuyafanyia kazi huku akiahidi kuwatuma mawaziri wa sekta husika waende kuyashughulikia.
“Nimeona zipo changamoto nyingi za wakulima na wafugaji zipo za viongozi wenu hawana magari nitakwenda kuangalia kwa waziri wa TAMISEMI nijue katika halmashauri hii kuna magari mangapi.
Nataka nijua kwa nini DC (Mkuu wa Wilaya) hana gari wakati anatakiwa kutembelea maeneo na kutatua migogoro. Nitatuma watu wangu waje kufanya uchunguzi wa kutosha nijue tatizo ni nini. Yale nitakayoyaweza nitayatatua," alisema.
AMTAKA JAFO MKURANGA
Baada ya kufika Mkuranga, pamoja na mambo mengine, alishtushwa na taarifa kwamba hakuna kituo cha afya licha ya kwamba serikali ilishatoa Sh. milioni 400 kwa ajili ya ujenzi.
Kutokana na hali hiyo, alimpigia simu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwenda leo kuchunguza kwa nini kituo hicho hakijajengwa.
“Nataka ufike kesho hapa ili upate majibu kwa nini hakuna kituo cha afya. Nataka uhoji fedha zimekwenda wapi na kama zimeliwa ni nani aliyekula,” alisema.
0
Comments
Sign in to post a message
You're the first to comment.
Say something
Recommend
Log in