Log inLog Out
EntertainmentRelationshipLifestyleSportTechnology
Kigwangalla azindua mpango mpya kukuza utalii wa ndani

Na Mwandishi Wetu

July. 03, 2020

Mkakati huo wenye kaulimbiu ‘Utalii Mpya, Fursa Mpya’ unaratibiwa kwa pamoja baina ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), kampuni ya Real PR Solutions ya jijini Dar es Salaam, BRAJEC, pamoja na kampuni ya Peak Performance.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ulihusisha na viongozi wengine waandamizi kutoka serikalini na pamoja na wadau wa utalii nchini wakiwamo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Chama cha watoa huduma za utalii wa ndani (TLTO) na Shirika la Hifadhi za Taifa  (TANAPA).
Wengine ni Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), viongozi waandamizi kutoka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Precision Air pamoja na wadau wengine.
Dk. Kigwangalla alisema mpango huo umekuja wakati mwafaka wakati ambapo serikali imejizatiti kuhakikisha sekta hiyo inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na wadau kutoka ndani ya nchi wakiwamo wawekezaji wadogo ili kutoa fursa za ajira na kutoa nafasi kwa wadau hao kushiriki kukuza sekta hiyo.
“Katika kufanikisha ushiriki wa wawekezaji wazawa hususani wale wadogo wadogo kwenye sekta ya utalii, serikali iliamua kushusha tozo mbalimbali na masharti ambayo yalikuwa kikwazo kwa wadau hao kushiriki kwenye sekta hii muhimu.”
Alisema uamuzi huo wa serikali umewezesha ongezeko kubwa la wadau hao kushiriki kwenye sekta ya utalii, kwa wa mwaka 2019 idadi ya wawekezaji kwenye sekta hiyo iliongezeka kutoka 1,100 hadi takribani 2,000 ambapo 600 kati ya hao ni wawekezaji wapya wazawa.
Mshauri Mkuu wa Mpango huo, Dk. Fenella Mukangara, alisema mpango huo unaohusisha juhudi mahsusi katika kusaidiana na serikali kukuza utalii wa ndani na kupunguza athari za janga la corona kwenye sekta hiyo muhimu.
Alitaja baadhi ya mambo muhimu kwenye kampeni hiyo ambayo yatatekelezwa kwa awamu kuwa ni mafunzo kwa vijana kote nchini ili waweze kunufaika na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii ikiwamo kuongoza watalii, mafunzo ya huduma kwa wateja katika hoteli na migahawa, vyombo vya usafiri na ujuzi wa kufungua kampuni za utalii.
"Tunatarajia mafunzo haya yatawanufaisha vijana zaidi ya 100,000 hususani wale wasio na ajira ili waweze kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii na wazitumie vizuri.”
Aidha, Dk. Mukangara alitaja mikoa itakayoanza kunufaika na mpango huo ni  Kanda ya Ziwa ikiwamo Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu, Mara na Shinyanga.
Alisema katika kuupamba mkakati huo kutakuwa na uhusishwaji wa matukio mbalimbali ya michezo na burudani ili kuvutia walengwa zaidi wa mpango huo. Matukio hayo ni pamoja na mbio za Capital Mountain Run zitakazofanyika katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Pia mdahalo wa masuala ya utalii na uwekezaji Kanda ya Ziwa (Lake Zone Tourism and Investment Symposium) utakaofanyika jijini Mwanza.
Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Dk. Costantino Bushungwa, alisema chuo kimejipanga kuhakikisha kinawaandaa kitaalamu wadau wa utalii ili waweze kutambua fursa zitokanazo na sekta hiyo muhimu na waweze pia kunufaika.
0
Comments
Sign in to post a message
You're the first to comment.
Say something
Recommend
Log in